
KATIKA siku za hivi karibuni nchi yetu imeonekana kugawanyika na hata kushindwa kufikia muafaka wa pamoja na maamuzi ya hiyari juu ya masuala muhimu yanayolikabili Taifa.
Karibu katika kila mjadala, uwe ni mjadala juu ya katiba ya nchi, bajeti ya taifa, sera na maamuzi ya kiserikali; au mjadala juu ya sheria mpya na zile zinazorekebishwa, Taifa letu limekuwa likigawanyika.
Cha kushangaza ni kwamba, katikati ya mgawanyiko huu, mara zote pande zinazosuguana iwe ni chama kilicho madarakani au upinzani, kila upande umekuwa ukidai kuwa unasimamia uzalendo na maslahi ya Taifa!
Kinachoshangaza zaidi ni kwamba “uzalendo ni kitu kimoja na maslahi ya taifa huwa hayagawanyiki”, lakini bado Taifa limekuwa likigawanyika katika makundi mawili au zaidi huku kila moja likidai kusimamia uzalendo na maslahi ya Taifa.
Mathalan, bila kuingilia uhalali wa kisheria na kikanuni, ni ukweli ulio dhahiri kuwa maamuzi mengi yaliyopitishwa na Bunge letu yamekuwa yakitegemea zaidi nguvu ya kura kuliko utashi na hiyari ya pamoja juu ya nini hasa tunakwenda kukisimamia au kukitekeleza kwa pamoja kama Taifa.
Upo msemo wa Kiswahili usemao “hiyari yashinda utumwa”. Kwa namna yoyote ile, maamuzi yanayotegemea zaidi shinikizo la kura chini ya utaratibu wa “wengi wape” kuliko kujenga hiyari na muafaka wa pamoja, hayawezi kuwa na afya wala tija ya kutosha katika kusukuma maendeleo ya Taifa.
Jambo lolote lile linalojengwa kwa hiyari ya pamoja huwa lina fursa zaidi ya kufanikiwa kuliko lile linalosukumwa katikati ya tofauti na migawanyiko mingi. Na ndiyo maana huwa tunasema “umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu”
Katika hali ya kawaida, kama kila mmoja angekuwa anasimamia kweli uzalendo na maslahi ya Taifa kwa usahihi na kwa uhakika, basi Taifa hili lisingegawanyika kamwe.
Tungekuwa kitu kimoja siku zote na kusukuma kwa pamoja maendeleo ya Taifa letu. Hata mgawanyiko uliojitokeza kwenye kushughulikia sakata la mchanga wa madini (makinikia), sheria na mikataba ya madini usingetokea.
Hali hii inaonyesha dhahiri kuwa kuna uelewa mdogo sana na mkanganyiko wa hali juu kuhusu nini hasa ni uzalendo na maslahi ya taifa; na nini hasa si uzalendo na si maslahi ya taifa.
Taifa lenye viongozi wasio na uzalendo ni Taifa linalokwenda mrama; na Taifa lenye raia wasio na uzalendo ni Taifa linalozama. Kama “maendeleo endelevu ya nchi” yangekuwa mithili ya “Gari linalotembea”, basi “uzalendo” ndio “mafuta yake”.
Leo inapofikia hatua nchi inagawanyika katika kuyajua na kuyapigania maslahi yetu kwa pamoja, basi hatuna budi kufanya tafakari ya kina juu ya namna bora zaidi ya kuutambua na kuuimarisha uzalendo wetu.
Kumekuwa na mitazamo na hoja potofu kuhusu uzalendo na maslahi ya taifa. Kupitia kauli za viongozi wengi wa kiserikali na kisiasa, mtazamo na tafsiri inayopandikizwa ni kuwa uzalendo ni kuunga mkono jambo lolote linalosemwa, kuamuliwa au kutendwa na viongozi wa kiserikali au serikali yenyewe.
Kwa mantiki ya dhana hii, anayekosoa, kupinga au kushauri kinyume na mtazamo wa kiserikali, huyo si mzalendo.
Mtazamo na tafsiri hii potofu kuhusu uzalendo unapandikiza fikra potofu kwa jamii kuwa viongozi wa serikali siku zote huwa hawakosei. Wanachowaza na kutenda kwaajili ya nchi ndiyo sahihi. Mtazamo huu potofu unawafanya binadamu wenzetu wanaoongoza serikali kupewa “hadhi ya umalaika” ambayo hawana.
Mtazamo na tafsiri hii potofu kuhusu uzalendo unapandikiza fikra potofu kwa jamii kuwa viongozi wa serikali siku zote huwa hawakosei. Wanachowaza na kutenda kwaajili ya nchi ndiyo sahihi. Mtazamo huu potofu unawafanya binadamu wenzetu wanaoongoza serikali kupewa “hadhi ya umalaika” ambayo hawana.
Kwasababu ya mtazamo huu potofu kuhusu uzalendo, baadhi ya viongozi wa kiserikali nao wamekuwa wakijiona kuwa wao ndio kielelezo na kipimo pekee cha uzalendo. Wenye mawazo au ushauri mbadala dhidi ya kile kinachofanywa na serikali, hao huonekana sio wazalendo.
Katika hali ya kusikitisha sana watu hawa huitwa “wajinga, waropokaji, wachumia tumbo, vibaraka au watu wanaotumika”, hata pale wanapokuwa wamekosoa na kupinga jambo kwa nia njema kabisa ya kuinusuru nchi yao.
Madhara ya tafsiri hizi potofu kuhusu uzalendo hayaishii tu kwenye kuwajengea chuki watu wema wanaokosoa na kupinga maamuzi na matendo mabaya ya serikali, bali pia yanavunja-vunja uhuru na utayari wa wananchi katika kuchangia kwa hiyari maono na fikra zao kwa maendeleo ya nchi yao.
Tusipokuwa makini nchi hii itajikuta inayumba na kuzidi kuporomoka kwasababu ya kulazimisha kutegemea fikra na matakwa ya upande mmoja pekee, huku ule mwingine ukijengewa chuki na ubaguzi kuwa hauna uzalendo
Kwa maneno mengine, tafsiri potofu kuhusu uzalendo inaweza kabisa kusababisha watu wasiwe wazalendo kwa nchi yao. Anayeona jambo baya linalofanywa na Kiongozi wa kiserikali, iwe ni rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka au utekelezaji mbaya wa sera na mipango ya nchi, anaweza kabisa kuamua kunyamaza.
Hatafichua mabaya yanayofanyika kwasababu tu akisema huenda akaitwa mjinga, kibaraka, anatumika na pengine vyombo vya dola vikaagizwa vimchukulie hatua.
“Fikra sahihi hujenga Taifa, na fikra potofu hubomoa Taifa”.
“Fikra sahihi hujenga Taifa, na fikra potofu hubomoa Taifa”.
Tukifanya mzaha, siku moja Taifa hili linaweza kujikuta limeanguka na kupasuka vipande vipande; si kwasababu hakutakuwa na fedha au raslimali za kuleta maendeleo, bali kwasababu fikra na dhana potofu zinazopandikizwa na viongozi kuhusu uzalendo, zitakuwa zimekamilisha kazi yake ya kuligawa Taifa katika vipande vipande vya chuki na ubaguzi na kubakisha watu wasio na utayari wala uhuru wa kuhoji, kukosoa, kupinga au kushauri chochote chema kwa maendeleo ya Taifa lao.
Uzalendo hauna maana nyingine yoyote ya msingi zaidi ya raia kuipenda, kuipigania na kulinda maslahi ya nchi yake kwa juhudi zake zote na kwa uaminifu usiotia shaka. Kwa mantiki hiyo, mzalendo wa nchi ni mtu yeyote yule anayetetea mambo mema na kupinga mambo mabaya yanayofanywa kwa nchi yake.
Ili nieleweke vema na pengine kuondoa ukakasi uliopo, ni vema nikasisitiza kuwa nchi siyo serikali. Kwa hiyo uzalendo hauna maana ya kuunga mkono kila linaloamuliwa au kufanywa na serikali, bali una maana moja tu ya msingi “kuipenda nchi yako”.
Kwa mantiki hii, kuikosoa na kuipinga serikali pale inapofanya mambo yanayoweza kudhuru nchi, ni uzalendo pia; na pengine huu ndio uzalendo wa hali ya juu maana Taifa huimarika zaidi kwa fikra zinazokosoa na kushauri kuliko kwa fikra zinazokubali na kubariki kirahisi-rahisi.
Rais wa zamani wa Taifa la Marekani, Mheshimiwa Theodore Roosevelt aliwahi kusema: “Patriotism means to stand by the country. It does not mean to stand by the President or any other Public Official” . Hapa alimaanisha kuwa “Uzalendo una maana ya kusimama pamoja na nchi yako. Haumaanishi kusimama pamoja na Rais au na Kiongozi mwingine wa Umma”.
Ni vema ikazingatiwa hapa kuwa Roosevelt naye alikuwa ni Rais, yaani Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, lakini kamwe hakupenda kupandikiza dhana potofu kuwa uzalendo ni kuunga mkono kile asemacho au afanyacho Rais.
Aliwaongoza wananchi wake katika ukweli, akiwataka wawe huru kuipenda na kuipigania nchi yao. Hakutaka kujenga uzalendo potofu wa “zidumu fikra za Rais”. Alitaka kujenga fikra sahihi za “yadumu maslahi ya nchi”.
Mkuu wa nchi yoyote ile si Malaika, ni Binadamu. Kama Rais anafanya jambo baya dhidi ya nchi au anakosea njia za kushughulikia mambo muhimu ya nchi, basi kwa mantiki ya Rooselt Rais huyo akosolewe, ashauriwe na apingwe ili maslahi ya nchi yatimie. Huo ndio uzalendo.
Lakini tukiufanya Urais kuwa ndio mnara wa uzalendo, basi mtazamo huo finyu unaweza kabisa kuangamiza maslahi ya taifa pale inapotokea binadamu aliyeshika cheo cha urais anafanya kinyume na maslahi hayo.
Kwa maneno mengine, Rais Mzalendo ni yule anayeweka uhuru na kuhamasisha raia wa nchi kuipenda na kuiheshimu nchi yao zaidi kuliko kufungwa katika mnyororo wa maono na maamuzi yake tu.
Rais mzalendo ni yule anayependa kukosolewa, kushauriwa na hata kupingwa kwa lengo la kupata muafaka wa pamoja na ulio sahihi zaidi katika kuyakuza na kuyalinda maslahi ya nchi.
Mmoja wa Wanaharakati maarufu duniani aliyepinga ubaguzi wa rangi na kupigania haki za watu weusi, Comrade Malcom X, alipata kusema: “You are not to be so blind with patriotism that you cant face reality. Wrong is wrong no matter who does it or says it”
Kwamba: “hupaswi kuwa kipofu sana wa uzalendo kiasi cha kushindwa kuukabili uhalisia. Kosa ni kosa tu, hailjalishi ni nani ametenda au amesema”
Wakati maana kuu ya uzalendo ni kuipenda nchi yako, tafsiri pana ya kauli hii ya Malcom X inatufundisha kuwa uzalendo haupo kwa lengo la kuwapofusha watu wasione hata mabaya yanayofanyika ndani ya nchi yao, hata kama yanafanywa na viongozi wakuu wa nchi.
Amesisitiza Malcom X kwamba “makosa ni makosa tu, haijalishi ni nani ametenda au amesema”. Kwa mantiki hiyo, katika kurutubisha uelewa na kuimarisha uzalendo wa Watanzania kwa nchi yao hakuna kitu muhimu sana kama kuwapa watu uhuru wa kukosoa na kupinga mabaya hata kama kimefanywa na wakubwa wa nchi.
Mimi naamini kama Watanzania wenzetu waliokuwa serikalini wakati nchi inaingizwa kwenye mikataba feki ya wizi wa madini wangekuwa na kiwango hichi cha uzalendo anachokizungumzia Malcom X, hichi cha kupinga uovu bila kujali ni nani anayeutenda, basi Tanzania yetu isingegeuzwa kuwa Shamba la Bibi kiasi hichi.
Lakini tumefika hapa kwasababu baadhi ya watu waliamua kuwa na nidhamu iliyopitiliza kwa wakubwa waliotuingiza kwenye mikataba feki. Pengine wakidhani nidhamu hiyo ndiyo uzalendo.
“Obedience is not Patriotism. Patriotism is love of your country, not your government”. Kwamba, “Utii si uzalendo. Uzalendo ni upendo wa dhati kwa nchi yako, si kwa serikali yako”.
“Obedience is not Patriotism. Patriotism is love of your country, not your government”. Kwamba, “Utii si uzalendo. Uzalendo ni upendo wa dhati kwa nchi yako, si kwa serikali yako”.
Hapa namaanisha kuwa nidhamu au utii licha ya kuwa ni mambo muhimu bado hayamaanishi kuwa huo ndio huo uzalendo. Utii au nidhamu unahusu kuheshimu mamlaka ya juu yako, lakini kufanya hivyo haina maana kuwa huo ndio uzalendo kwa nchi.
Inapotokea mamlaka yako ya juu imefanya au inakusudia jambo linaloweza kudhuru nchi yako, basi utii na nidhamu havipaswi kumfunga mtu hata ashindwe kukosoa, kushauri au kufichua uovu huo kwa maslahi ya Taifa, maana kufanya hivyo ndio uzalendo wenyewe.
Uzalendo hujengwa. Mtu hazaliwi akiwa anaipenda Tanzania na kuwa tayari kuifia nchi yake, bali hujengwa kiakili na kisaikolojia katika kuitambua vizuri nchi yake, kuipigania na kuilinda.
Lakini ukifuatilia jinsi uzalendo wa nchi hii unavyojengwa utakuta kinachofanyika sana ni kuwafundisha wanafunzi kuimba wimbo wa Taifa, kuitambua bendera ya nchi, historia ya nchi na zaidi kukimbiza Mwenge.
Sibezi jitihada hizo, lakini ni ukweli kuwa mtu hawezi kuipenda nchi yake kikamilifu eti kwasababu tu amefundishwa wa Taifa na kukimbiza Mwenge. Hii haitoshi.
Msingi mkuu kuliko yote ya kujenga uzalendo wa wananchi kwa nchi yao ni kuhakikisha serikali inatenda mambo mema kwa watu wa Taifa hili. Kinyume na hapo wananchi hawawezi kuwa na uzalendo kwa nchi yao.
Msingi mkuu kuliko yote ya kujenga uzalendo wa wananchi kwa nchi yao ni kuhakikisha serikali inatenda mambo mema kwa watu wa Taifa hili. Kinyume na hapo wananchi hawawezi kuwa na uzalendo kwa nchi yao.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema, nanukuu, kwamba “uhalali wa serikali yoyote ile iliyopo madarakani hautokani tu na katiba au sheria iliyoiweka serikali hiyo madarakani bali unatokana na matendo sahihi na mema ya serikali hiyo kwa watu wake.
Ni vema ikazingatiwa hapa kuwa uhalali huu wa serikali ambao Mwalimu alisema unapatikana zaidi kwa kuwatendea mema wananchi, ndio huo huo wenye uwezo wa kujenga na kuimarisha uzalendo wa wananchi kwa nchi yao.
Katika nchi ambayo watu hawapati haki na stahili zao ni vigumu kupata wananchi wenye uzalendo wa kutosha. Wananchi wenye shida ya maji, pembejeo za kilimo, uhaba wa zahanati na madawa na shida za mitaji ya kufanyia biashara kwa mfano, wataipenda vipi nchi yao ikiwa serikali yao haitimizi wajibu wake?
Hivi wananchi wanaobomolewa nyumba zao bila kupewa fidia, wataipenda aje nchi yao kwa uonevu na ukatili wanaofanyiwa!!
Serikali inayoonea na kunyanyasa raia inawafanya raia hao wawe ni wazalendo wa kupigania haki zao binafsi zaidi na kusahau hata umuhimu wa kuipigania nchi.
Imeandaliwa na Mchungaji Peter Msigwa
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.