
Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi ameliagiza baraza la madiwani la halmashauri ya Wilaya Kilwa kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo Zabron Bugingo kulipa deni la michango ya Saccos za walimu wa wilaya hiyo zilizotumika na halmashauri hiyo na kusababisha walimu kutoweza kukopeshana kutokana na michango na makato yao ya mishahara.
Zambi ametoa agizo hilo katika kikao cha robo ya pili ya mwaka cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kufuatia halmashauri hiyo kutolipa deni hilo kwa kipindi kirefu na kusababisha walimu kushindwa kukopa kupitia chama chao cha kuweka na kukopa licha ya maagizo mengi kutolewa nae pamoja na naibu waziri wa Tamisemi.
Aidha Zambi amebainisha kuwa kutolipwa kwa deni hilo atachukua hatua za kuzuia vikao vya kamati za madiwani pamoja na baraza lijalo ili kuhakikisha walimu wanapata stahili zao ili walimu hao wawe na ari ya ufundishaji kuondokana na ufaulu mdogo wa wanafunzi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Abuu Mjaka alikiri kupokea agizo hilo na kubainisha kuwa licha ya halmshauri hiyo kuwa na madeni makubwa tayari wamejipanga kulipa deni hilo na madeni mengi huku Mkurugenzi wa halmshauri hiyo Zabron Bugingo alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa uwepo wa deni hilo ambapo alibainisha kutoa taarifa za deni hilo kupitia vikao vinavyofuata.
Nae Abdallah Hemed Mkumbaru diwani wa kata ya chumo akiongea baada ya kumalizika kwa kikao hicho alieleza kuwa pamoja na uwepo wa madeni mengi tayari wamejipanga kwa ukusanyaji wa mapato baada ya kuanzisha vyanzo vipya vya makusanyo.
Zaidi ya shilingi milioni 40 zinadaiwa na walimu wa wilaya hiyo katika kipindi kilichoanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2016 hali iliyochangia walimu kumuomba mkuu wa mkoa kusimamia ulipajwi wa deni hilo ili walimu waweze kujiendeleza kwa mikopo inayotokana na mishahara yao.
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.