Dodoma. Serikali imeionya Manispaa ya Mji wa Kigoma Ujiji kuacha kuendelea kuwasiliana na Mpango wa Kuendesha Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) na kama itaendelea itachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuvunja baraza la madiwani.
Serikali ilijiondoa katika mpango huo Septemba, ikieleza kuwa sababu ni kuwapo kwa Sheria ya Upatikanaji wa habari ya mwaka 2016 inayolenga kuongeza upataji wa taarifa na uwazi wa shughuli za Serikali.
Hata hivyo, jana imeitaka Kigoma Ujiji kuachana na mpango wa kuwasiliana na OGP.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alisema hayo bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe ambaye chama chake kinaongoza manispaa hiyo.
Katika swali lake la nyongeza, Zitto alisema nchi za Hungary na Urusi ambazo Serikali inasema zimejitoa katika mpango wa OGP ni miongoni mwa mataifa yanayooendeshwa kidikteta kwa kutofuata utawala bora. “Nchi za Hungary na Urusi zinaendeshwa bila kufuata demokrasia, zinaendeshwa kidikteta ni aibu sana kwa Serikali kusema inaiga nchi ambazo zinaenda kinyume na demokrasia,” alisema.
Alisema majukwaa hayo ya kimataifa yanatengeneza uhusiano na kwamba, Canada ni mwenyekiti wa mpango huo. Hata hivyo, alisema juzi ameona Rais John Magufuli amemwandikia waziri mkuu wa Canada kuhusu suala la Bombardier. “Serikali haioni kwamba ingeendelea kuwa mwanachama wa OGP na mwenyekiti ni Canada hili ombi lingeshughulikiwa kwa uzito zaidi,” alihoji Zitto.
Alisema Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa miji 15 duniani ambayo iko katika mpango huo na kuitaka Serikali kutoa kauli juu ya ushiriki wa mji huo katika OGP ambayo imekuwa ikifaidika na mpango huo na miji mingine inayotaka kuingia katika mpango huo.
Akijibu hayo, Mkuchika alisema Tanzania imejitoa katika mpango kwa hiari yake yenyewe na hawajaiga nchi yoyote. “Sisi ni Taifa huru linalojitawala, linalofanya matumizi yake yenyewe bila kushurutishwa na Taifa lolote liwe dogo ama kubwa duniani,” alisema.
Alisema Canada na Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Madola na pia Tanzania ina ubalozi wake na hivyo kuwa mwanachama wa OGP na kutokuwa mawasiliano na nchi hiyo haiwezi kuwa tatizo.
Mkuchika alisema andiko la mpango huo linasema nchi ikijiondoa uanachama na washirika wake wote shughuli na uanachama unakoma.
Hata hivyo, alisema Serikali ina taarifa kuwa Manispaa ya Kigoma Ujiji bado inaendelea na mpango huo na OGP walimwandikia waziri wa Mambo ya Nje kuwa bado wana nia ya kuendelea na halmashauri hiyo.
“Sasa (Spika) nataka kupitia Bunge lako tukufu kuionya Manispaa ya Ujiji kutoendelea. Nchi inayozingatia utawala bora haiwezi Serikali kuu ikafanya maamuzi lakini baraza la madiwani likasema haliwezi kutekeleza. Nataka nionye Halmashauri ya Kigoma Ujiji iache mara moja. Yale ni maamuzi ya Serikali na wakiendelea kufanya mawasiliano kama wanavyofanya sasa Serikali itachukua hatua kali za kisheria na nyinyi mnajua kwenye baraza la madiwani hatua kali za kisheria ni kulivunja baraza na kuunda Tume ya Manispaa,” alisema.
Mkuchika aliomba madiwani na Zitto kutoifikisha Serikali huko. Katika swali lake la msingi, Zitto alihoji kwa nini Serikali imeamua kujiondoa kwenye mpango huo. Akijibu Mkuchika alisema imejiunga na mipango mbalimbali ya kikanda na kimataifa itakayoijengea misingi imara ya uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi, kuongeza uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.